01.   Maana ya Jumuya Ndogo Ndogo ya Kikristo (JNNK)

Ni muungano wa familia za kikristo za kikatoliki kwa ujirani wao kuanzia familia mbili hadi kumi na mbili zinazokutana pamoja angalau mara moja kwa wiki kwa muda wa saa moja kushirikiana katika kusali, kusoma Neno la MUNGU na kulitafakari pamoja kujadili na kushirikiana katika mambo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kulingana na mazingira yao kwa madhumuni ya kumtafakari MUNGU na kuuishi ukristo wao kivitendo ili kuwa watakatifu.

02.   Idadi sahihi ya kaya zinazoweza kuunda Jumuiya

Idadi sahihi kabisa, kama vile joto la mwili wa mwanadamu ni nyuzi joto 37, idadi ya kaya inapaswakuwa 12.  Ishara ya makabila kumi na mbili ya Taifa la MUNGU na mitume Thenashara.  Namba 12 inautajiri mwingi kimaandiko: Watoto wa Yakobo walikuwa 12 nao ndio waliounda taifa la MUNGU. Hivyo makabila kumi na mawili, ndio msingi wa jumuiya ya MUNGU.  YESU aliteua Mitume 12, ili waunde taifa jipya la MUNGU.  Hivyo nasi leo, JNNK ni taifa la MUNGU mahalia, idadi ya kaya inayounda zinapaswa kuwa12, yaweza kukua, ila idadi isipitilize 24, maana yake  hapo tutakuwa tumeshapata  taifa/ jumuiya ya pili, yaweza kuwa pungufu, na hapo itaalikwa kwa namna ya pekee kuinjilisha ili idadi yake ifikie 12.  Jumuiya ikiwa na kaya chache yaani 12 hakutakuwa na kutegeana, wala ubaridi.

03.   Faida ya JNNK kwa mkristo mkatoliki

Faida za JNNK kwa mkatoliki ni nyingi, ni vigumu kuzielezea zote kwani kila mmoja inamgusa kwa namna yake.  Zifuatazo ni fadida chache.

a.    Kwa mtu binafsi: inamsaidia mkristo kukua kiroho na kutatua matatizo yake kuishi furaha zake pamoja na wenzake, yaani kukua kimahusiano.  Inamsaidia mkristo kuwa na upeo mkubwa wa kiroho hasa anaposhirikiana na wenzake tafakari mbalimbali.  Inamsaidia mkristo kujisuta wenyewe kwani kutokana na udogo wake wote wanapata kujuana na kuhusiana kwa karibu.

b.   Kwa kaya:  Kushirikishwa katika masuala ya kiroho. Inasaidia kaya kuishi maadili ya kikiristo hasa, inavyoshirikisha kaya nzima baba, mama, watoto na ndugu wanaoishi nao hivi wanakuwa na nguvu ya kuishi pamoja.  Inasaidia ukuzaji wa Imani ya wanakaya.

c.    Kwa Kania:  Inasaidia kuimarisha uhai wa Kanisa.  Kwani matendo ya Kanisa yaweza kuonekana Zaidi katika JNNK kuliko katika ngazi za juu za Kanisa.  Ni kioo cha uhai wa Kanisa, kwani Kanisa lililo hai ni lile lenye Jumuiya hai.  Uinjilishaji wa kina wa Kanisa hufanywa hapa kimatendo.

d.   Kwa jamii:  Hutoa msaada wa kijamii kwa watu wanaoizunguka bila kujali kama ni wakristo au la.  Ni chumvi kwa jamii nzima inayowazunguka.  Hata wasio wakristo wanaguswa.  Ni mfano halisi wa umoja na ushirikiano kati ya Wakristo na watu wengine.

Mtakatifu Papa Yohane Paulo alisema haya juu ya tabia ya JNNK:
       
“… kwanza lazima ziwe sehemu za kujishughulisha na kujitangazia injili yenyewe, ili nao waweze kuwaletea Habari Njema wengine; Zaidi ya hayo lazima jumuiya ambazo huomba na kusikiliza Neno la MUNGU, kuhimizana kwa washiriki wenyewe kuchukua wajibu, kujifunza kuishi maisha ya kikanisa na kutafakari juu ya shida mbalimbali za kibinadamu katika mwanga wa kiinjili.  Zaidi ya yote Jumuiya hizi lazima ziishi maisha ya upendo wa KRISTO kwa wote, upendo unaopita mipaka ya muungano wa ukoo, makabila au vikundi vingine.”
Hivyo, mkristo yeyote anayetaka kujua faida ya Jumuiya shiriki kikamilifu na kwa udumifu maisha yake, utaona uhondo wake kama vile waswahili wasemavyo kuwa ukitaka kujua uhondo wa ngoma, ingia ucheze.

04.  Ukaaji katika Jumuiya wakati wa mkutano wa sala
Mkao wake mzuri na unaohimizwa unapaswa kuwa wa duara.  Wanajumuiya wote waonekane.Hii ni muhimu sana kwani katika kushirikishana neno kutakuwa hakuna kutegeana, wala ubaridi.  Ili kuweza kufanya duara hili, ni vigumu kama Jumuiya ina kaya zaidi ya 12.Mkao katika Jumuiya usiwe kama ule ukaaji wa kanisa, la hasha, bali uwe kimduara ili kila mwanajumuiya aonekane vizuri katika kuleta ushiriki hai.  Muda wa sala katika Jumuiya unatakiwa uchukue saa moja tu na si zaidi ya hapo.  Pia, wanajumuiya wanatakiwa kupanga muda wa kukutana ambao utawawezesha wanajumuiya wengi kuweza kushiriki bila vipingamizi.  Mfano wanaweza kukutana kila Jumamosi asubuhi kuanzia saa 12:30 hadi saa 1:30 asubuhi.

05.   Maji ya Baraka kwenye Jumuiya

Ni vizuri wakati wa kusanyiko la sala kwa wanajumuiya, kuwepo na Maji ya Baraka yanayowekwa mahali pazuri panapoonekana vizuri, na wanajumuiya wenyewe wanapofika wanaweza kuchovya vidole katia Maji ya Baraka na kujibariki, kama ishara ya kukumbuka ubatizo wao, na hivyo kukiri kwamba sisi sote tuliopo hapa ni ndugu moja, tumejumuishika kutokana na ubatizo wetu mmoja.

06.  Msalaba

Kila Jumuiya inatakiwa kuwa na Msalaba wenye mwili uliobarikiwa, ili kila wanajumuiya wakutanikapo kwa sala msalaba huo uwepo na uwekwe katikati ya kusanyiko, yaani katikati ya mduara uliofanyizwa na ukaaji wa wanajumuiya.

Hebu tutazame kwa ufupi uhusiano wa msalaba na JNNK

Msalaba unajengwa na mbao mbili, moja yatoka kulia hadi kushoto na ya pili yatoka chini hadi juu.  Mbao inayotoka chini hadi juu ni kiwakilishi cha uhusiano wetu na MUNGU, na ubao utokao kulia hadi kushoto unawakilisha uhusiano wetu na jamii, na majirani zetu.  Mbao mbili za msalaba zinafanana na Mbao mbili alizopewa Musa (Kut. 32: 15 na kuendelea).  Mbao mbili za Torati, ubao mmoja ulikuwa na amri ya kwanza mpaka ya tatu.  Ni amri zinazoelekeza uhusiano kati ya mwanadamu na Muumba wake.  Ubao wa pili ulikuwa na amri ya nne hadi yak um, zinazoelezea uhusiano wa mtu na mtu.

Mkusanyiko wowote wa kijumuiya una mambo haya mawili, tunakusanyika majirani na mkusanyiko wetu ni wa kumsifu MUNGU.  Mkusanyiko wa JNNK ambao MUNGUsi kilele chake, mkutano huo hauna tofauti yoyote na asasi isiyo ya serikali.  Na kama mkusanyiko wetu kwa ajili ya kumsifu MUNGU, bila kumjali jirani, huo ni unafiki mtupu.  Kuna hatari ya JNNK kuwa ni unafiki mtupu au kuwa ni asasi isiyo ya serikali, ndio maana lazima kila mnapokutana muwe na msalaba katikati yenu uwakumbushe wito wenu.  Tukumbuke:  “Mtu akisema anampenda MUNGU, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda MUNGU ambaye hakumwona” (1 Yoh 4:20).

Msalaba wa KRISTO ni sadaka, na bila sadaka maisha ya JNNK hayawezekani.  Kila mmoja anapaswa kujitoa sadaka kwa ajili ya mwenzake.

Mfano, Ndugu Muda, yeye hawezi kwenda katika Jumuiya kwa sababu hana muda.  Kazi zake zinambana mmno, toka Dominika hadi Dominika.  Lakini mtu huyu huyu ana nafasi ya kutazama tamthilia au mechi za mpira wa miguu katika luninga, katika vikao vya harusi yeye ndiye wa kwanza kufika ili kamati zikiundwa achaguliwe katika kamati ya vinywaji na kila siku hakosekani katika baa.  Ukimwambia hili atakujibu kule naenda kupunguza mawazo kidogo.  Lakini muda wa kuondoa uzito wa ubinafsi hana!

Ndugu Muda, kama kweli MUNGU ananafasi katika moyo wake, nina uhakika atapata muda wa kushiriki ibada katika JNNK.  Inafaa pia kuwaomba wanajumuiya wenzako kurekebisha mara moja moja ratiba ili kumuwezesha yeye naye kuwa hai pamoja na wanajumuiya wenzake.

Ndugu Michango, yeye amechoshwa na michango katika Jumuiya.  Alinihesabia, mchango wa maendeleo ya kanisa, mchango wa ujenzi wa choo, mchango wa shilingi 10,000 kwa kila mbatizwa kwa wtu wakubwa na shilingi 5,000 kwa kila mbatizwa mtoto, mchango kwa ajili ya mwanajumuiya aliyelazwa na bado kwa kila Dominika kuna sadaka mbili hadi tatu.

Kwa kweli hapa lazima tujiulize swali moja tu, je, michango hii yote ni kwa ajili ya kuchezea Kamari au kwa ajili ya ulevi?  Je, tukisha ikusanya michango hii tunakwenda kutupa chooni?  Kama ni michango kwa shughuli zenye umuhimu kwa ajili ya kuwapatia jirani zetu ukarimu wa KRISTO, kuendeleza na kuleta ustawi wa maendeleo ya parokia, hatuwezi kuepukana nayo.  Tunatakiwa kutoa kwa moyo na kwa furaha kulingana na uwezo wa kila mtu.

Wahenga walituasa, kidole kimoja hakivunji chawa!  Hatuwezi kuushinda uovu katika ubinafsi wetu, kwa kushirikiana pamoja ndani ya Jumuiya twaweza kabisa kumshinda adui yetu shetani.  Hivyo, tujitahidi sana kadiri tuwezavyo kuvishinda vikwazo vyote vinavyo tuzuia tusishiriki Jumuiya.  KRISTO mwenyewe ametuonesha njia, kwa kutanguliza kwanza mapenzi ya BABA, na si kutanguliza matumbo yetu au furaha zetu, malimwengu upitao kama upepo wa kisurisuri.

07.   Je, ni masomo gani yanayofaa kusoma kwenye Jumuiya?

Endapo wanajumuiya wameamua kusoma masomo ya Dominika inayofuata, ni vizuri kama ni lazima kusoma somo la Injili, kwani ndio tui na kilele cha masomo yote.  Ila tu tukumbuke kuwa Maandiko Matakatifu yote toka kitabu cha Mwanzo hadi cha ufunuo, yafaa kwa kutuongoza katika njia iliyo nyofu. (2 Tim 3:16).

Pia, wanajumuiya wanaweza kusoma somo linaloendana na hitaji la Jumuiya.  Mfano wanajumuiya wakienda kumtembelea mgonjwa au wanataka kuombea wagonjwa, wanaweza kusoma somo linaloelezea YESU akiponya wagonjwa n.k.

08.   Ni nani atoe tafakari ya Injili au somo lililosomwa?

Kwanza ni vizuri tufahamu kwamba tunapozungumzia Jumuiya tunazungumzia ushirikiano, hivyo hata katika ibada zetu twatenda pamoja.  Hivyo si sahihi kusema nani aongoze tafakari.   Nimewahi kukutana na mtu ambaye hakuwa anaenda kusali na wenzake, na tatizo lake ni kuwa hakuwa na uwezo wa kuongoza tafakari, hivyo aliogopa kwani siku itakapokuwa zamu yake, angelazimika kuongoza pasipo kutaka.  Au unakuta Jumuiya kila siku ya kukutana ni Mwenyekiti au Katibu wa Jumuiya ndiye anayeongoza tafakari na kama hayupo siku hiyo tafakari haipo!!

Kila mmoja wetu baada ya kusikia somo mara mbili, yafuatayo yaweza kumwongoza katika tafakari yake binafsi moyoni, kabla hajawashirikisha wenzake:

·         Je, somo nililolisikia limenigusa nini mimi moyoni mwangu? Kitu ambacho uliposikia tu, kilifanya nafsi yako, igundue kitu kipya, katika mahusiano yako na MUNGU, mwenzako wa ndoa, wanakwaya wenzako na jirani kwa ujumla.  Ni sawa na mama yule aliyekuwa anamsikiliza YESU, aliguswa na neno lake ndio maana alipaza sauti yake na kusema:  “Heri mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha” (Lk 11:27).  Mama huyu aliguswa na Neno Lake.

·         Somo nililolisikia limenisaidiaje?  Mimi kama mimi nimejitambuaje, nina uwezo au mapungufu gani, sijatimiza wajibu wangu?  Je, somo hili limenisutaje nafsini mwangu?  Tusiachie tu kuwa limenigusa, baada ya kunigusa, limekuelekeza katika changamoto gani ya kuyafanya maisha yako yawe bora Zaidi.  Hili ndilo lililowatokea watu wa Yesurusalemu baada ya kusikiliza hotuba ya Petro, waliuliza: “Ndugu zetu, tufanye nini?” (Mdo 2:37).

·         Nimebadilishwaje na somo hili ambalo limenigusa, limenisaidia, na sasa napaswa kutenda jambo Fulani kama mwitikio wangu kwa hilo neno.  Wengi wetu tunapenda kuishia na kuguswa tu, wachache tu tunaruhusu neno hilo kuwa la msaada katika maisha yetu.  Hatua hii ya tatu ni ya utendaji: “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si kuwa wasikilizaji tu …” (Yak1:22).  Zakayo mtoza ushuru anatufundisha juu ya hatua hii kwa kauli aliyoitoa mbele ya kadamnasi iliyokuwa ikimfuata YESU: “Sikuliza BWANA! Mimi nitawapa masikini nusu ya mali yangu, na kama nimemdanganya mtu yeyote kitu, nitamrudishia kiasi hicho mara nne” (soma Lk 19: 1-10).

Hivyo tukisha lisikiliza neno, kila mmoja wetu ananafasi ya kutushirikisha nini kilichomgusa katika somo hilo, amesaidiwaje na somo hilo na hasa atuambie atatenda nini kulinga na changamoto aliyoipata kutokana na somo hilo.  Hivyo, tafakari ni tendo ni tendo lenye hatua tatu katika kutusaidia kuishi ushuhuda wa Habari Njema.  Hivyo hakuna mwanajumuiya ambaye anaweza kudiriki kusema kwamba yeye hawezi kushiriki tafakari, labla kama ameamua kwa makusudi kufunga masikio ya moyo wake.  Neno la MUNGU lenyewe lina nguvu kutugusa, kutuelekeza, kutupongeza, kutuonya na kutubadilisha, kama alivyosema Nabii Isaya: “Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni wala hairudi huku; bali huinyeshea ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa change; halitarudi bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma” (Isa 55:10-11).

09.   Kugawa Jumuiya

Kuwepo kwa kaya nyingi katika JNNK na kisha wachache tuwakawa wanashiriki katika Ibada ni dalili ya watu kuona ni vigumu kuendesha JNNK katika wingi huo.

Kugawa Jumuiya kigezo ni kimoja tu ni eneo wanaopakana kaya 12 ziunde JNNKmoja.  Kuna sehemu nyingine tatizo kubwa kwao la kugawa Jumuiya yenye kaya zaidi ya 24, ni kuangalia  nani anapochi nene, nani anatoa michango mikubwa kunapokuwepo na hitajiko.  Kama waamini watakuwa na mtazamo huu, wajiulize mara mbilimbili, Ukristo wao ni pesa au Imani yao?  YESU alituasa: “… Hamwezi kumtumikia MUNGU pamoja na mali” (Mt 6:24).

Angalisho hapa ni kuwa tendo la kugawa JNNK lisiwe la pupa tu, badala ya mgawanyo huu kuimarisha ushiriki wa wanajumuiya, ukawa chanzo cha kufa kwa JNNK.  Kwamba hata wale wachache waliokuwa wanasuasua kufika nao mkawavunja moyo.  Hivyo uelimishwaji unapaswa kufanyika, na sala kumwomba ROHO wa KRISTO, ambaye ni ROHO wa umoja, awaongoze katika nia yenu njema, inapaswa kusaliwa.

10.    Mwongozowa kuratibu shughuli za JNNK
Mara nyingi na sehemu nyingi, waamini wanapenda kuwa na Mwongozo wa kuendesha Mkutano wa sala kwa kila wanapokutana wenye kufanana kwa Jumuiya zote.  Jambo hili ni la muhimu sana, ila hapa kuna angalisho la msingi kabisa.  Mwongozo huu uwe katika mambo machache ya msingi, usitake kutoa maelekezo kwa kila kitu.  Hili ni la muhimu kwa sababu JNNK ndio chemchemi ya uhai wa Kanisa. Chemchemi ni eneo tete ambalo halipaswi kusumbuliwa na mizigo ya sheria, kwani kuna hatari ya kukausha ubunifu.  Ni katika JNNK pekee utamadunisho wa kweli waweza kutokea, na ili uweze kutokea zinapaswa kuachiwa uhuru katika mambo kadhaa, tena ya msingi tu.  Tuzingatie kwamba: “… na pale palipo na ROO wa BWANA ndipo ulipo uhuru” (2 Kor 3:17).

Nitoe mfano mmoja, katika mwongozo wa utaratibu wa sala, twaweza kusema kila juma kuwepo na ibada ya JNNK, na iwe angalau kwa muda wa saa moja.  Nini cha kufanya katika muda huo wa saa, hapa JNNK inapaswa kuwa huru kwa chaguo mbalimbali na kwa ubunifu.  Mambo ya kuzingatia ni uwezo wa wanajumuiya, uwingi wao, mahitaji yao kwa siku hiyo ya ibada, ni kipindi gani cha kalenda ya kiliturujia na eneo wanalokutanika.

Kuna mambo ambayo kwa kila ibada yatakuwepo:  kujuliana hali, kupeana majukumu na sadaka.  Lakini kuna mambo ambayo wanajumuiya wanaweza kuyanyambulisha ambayo watayaingiza katika yale ambayo ni ya kila siku:

                        i.        Kutafakari Injili, ama kuanza kusoma Injili na kurudia mara mbili baada ya ukimya na kila mtu kusema imemgusa vipi katika maisha yake au kusema tukio lililokugusa katika juma hilo na wanajumuiya kujaribu kuona Maandiko Matakatifu yanatoa mwanga gani wa kuelewa au kuitikia changamoto ya tukio hili.

                      ii.        Kama ni mwezi wa Mbarikiwa Bikira MARIA wanaweza kusali Rozari.  Napo kuna njia mbili, kusali Salam MARIA kumi baada ya kila fungu la rozari, ama kusoma sehemu ya Injili inayoelezea fungu husika.

                    iii.        Kama ni wakati wa Kwaresma, wanajumuiya baada yay ale ya kawaida, wanaweka katikati yake sala ya Njia ya Msalaba.

                     iv.        Kama siku hiyo wanamtembelea mgonjwa wanaweza kusali Ibada ya Wanajumuiya kwa Mgonjwa.

                       v.        Kama kuna ubatizo unaotolewa katika Jumuiya wanaweza kuamua kusoma katika Katekesimu ya Kanisa Katoliki, Kanisa linafundisha nini juu ya sakramenti hiyo.  Kitabu hiki ni cha muhimu sana  katika Imani yetu, ukitoa Biblia Takatifu naweza kudiriki hiki chafuatia kwa umuhimu.

UTARATIBU WA JUMLA

a)    Kwa jina la BABA…

b)   Wimbo wa Mwanzo
Unaweza kuwa wimbo wa kumwalika ROHO MTAKATIFU au wimbo wowote unafaa kulingana na kipindi cha Kalenda ya Kiliturujia.

c)    Kujuliana hali
Wanajumuiya wanajuliana hali kamawote ni wazima au kuna mgonjwa kati yao ili waweze kumwombea katika sala na maombi yao n.k.

d)   Somo
Somo lililoandaliwa linasomwa kwa mara ya kwanza kwa taratibu, kwa uchaji na kwa sauti inayosikika na wanajumuiya wote

e)    Ukimya Mtakatifu
Kisha somo kusomwa kwa mara ya kwanza, unafuata ukimya mtakatifu ili wanajumuiya walitafakari somo kwa kimya ili kuona somo limemgusa kiasi gani na ninatoa changamoto gani katika maisha yake.  Ukimya huu waweza kuwa dakika tatu hadi tano.

f)     Kurudia kusoma somo lile lile kwa mara ya pili
Somo linarudiwa kusomwa kwa sauti ya kusikika.  Si lazima mtu yule yule aliye soma kwa mara ya kwanza kurudia kusoma.  Mtu mwingine aweza kusoma.

g)    Kushirikisha tafakari
Kila mtu atoe tafakari jinsi ambavyo somo limemgusa katika maisha yake na kusema tukio lililomgusa katika juma na somo limempa changamoto gani katika maisha yake na linamtaka afanye nini.


h)   Maazimio
Kutokana na changamoto za somo, au mahitaji ya Jumuiya, wanajumuiya wanaweza kwa pamoja kuweka maazimio ya shughuli au majukumu ya kuyafanyia kazi kwa wiki inayofuata kabla ya mkutano mwingine wa sala.

i)     Maombi
Wanajumuiya wanaalikwa kutoa maombi mbalimbali kulingana na mahitaji ya mtu binafsi, familia, Jumuiya, Parokia, kanisa kwa ujumla na marehemu waliotutangulia.  Muda wa maombi utazamwe kwani kila mwanajumuiya akitoa ombi lake na kila ombi likichukua muda mrefu, inaweza kuchukua muda mwingi. Maombi yatolewe kwa ufupi na kwa ufasaha.

j)     Kukiri Imani
Wanajumuiya wanakiri Imani (Sala ya Nasadiki)  v  kwa pamoja.

k)   Mchango
Baada ya maombi, unafuata mchango (sadaka- kama tulivyozoea kuita).

l)     Matangazo
Kisha Mchango, kutolewe matangazo mbalimbali.  Matangazo haya pia yanatakiwa kutolewa kwa ufupi ili muda mwingi wa sala usichukuliwe na matangazo

m) Ibada ya kukabidhi Msalaba Mtakatifu familia nyingine

Mwenyekiti / Kiongozi wa Jumuiya:    Tumsifu YESU KRISTO!  Ndugu zangu katika KRISTO, napenda kuwajulisha kuwa leo tutakabidhi Msalaba Mtakatifu kwa familia ya Ndugu…
Somo: Hesabu 21:4-9
Wakasafiri toka mlima Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu, ili kuizunguka nchi ya Edomu:  watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia.  Watu wakamnung’unikia MUNGU na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani?  Maana hapana chakula, wala hapana maji na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.  BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.
Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia MUNGU, na wewe; utuombee kwa BWANA, atuondolee nyoka hawa.  Basi Musa akawaombea watu.  BWANA akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, atazamapo, ataishi.  Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.
Neno la BWANA  (W). Tumshukuru MUNGU.
Kiongozi wa Jumuiya: Ee MUNGU Mwenyezi na mkarimu, utuangaze kwa wema, sisi tuliokusanyika hapa, kutambua upendo wako kwetu.  Utujalie moyo wa kudumu katika Imani, Matumaini na Mapendo na kama ulivyokuwa kule Jangwani yule nyoka wa shaba aliyewekwa juu ya mti, na walipomtazama, wakaponywa na sumu ya nyoka, tunakuomba sote tutakaomtazama YESU aliyetundikwa msalabani kwa Imani kuu, tuponywe na sumu yote ya yule mwovu shetani. Tunakuomba utuimarishe kiimani.  Tunaomba hayo kwa njia ya KRISTO BWANA wetu.  Amina.
Kisha sala hiyo, maandamano ya kusindikiza Msalaba Mtakatifu ynaanza hadi kwenye kaya ambayo utafanyikia mkutano mwingine kwa wiki inayofuata, huanza mara moja wanajumuya wpte wakiandamana kwa furaha wakiongozwa na Msalaba.  Wifikapo mahali husika Kiongozi au mwanajumuiya yeyote aliyeandaliwa atanyunyizia sehemu ya nyumba ya wanafamilia maji ya Baraka na wanajumuiya wananyunyiziwa maji hayo huku wimbo ufaao ukiimbwa kwa furaha.  Baada ya tendo hilo, wanajumuiya wanatakiana Amani na kumalizia kwa sala ya   “Tunaukimbilia…” Kisha: Mtakatifu … Somo wa Jumuiya yetu utuombee.

Mwenyekiti / Kiongozi:  Nendeni na Amani
Wanajumuiya wote:  Tumshukuru MUNGU.
Kisha wanajumuiya wote wanatawanyika kwa furaha wakimtukuza MUNGU na kwenda kuliishi lile Neno walilolisikia na kutekeleza wajibu waliopangiana kama upo kwa sifa na utukufu wake MUNGU ili wanadamu waupate wokovu kwa njia ya KRISTO BWANA wetu.


Post a Comment

 
Top