02 / 02/2014

Somo I: Mal. 3: 1- 4
Somo II Ebr. 2: 14- 18

Injili Lk. 2 : 22- 40

      WAZO KUU: YESU NI FARAJA YETU

Utangulizi :(Kabla ya kubariki mishumaa nje ya Kanisa)
    Ndugu wapendwa, tumekusanyika hapa kuadhimisha kutolewa Bwana Hekaluni. Kadiri ya sheria ya Wayahudi kila mtoto wa kwanza alihesabika kuwa mali ya MUNGU, ilitakiwa atumike hekaluni. Ili kumfanya mtoto awe huru tena, yaani, mali ya wazazi ilipasa kumkomboa mtoto. Basi leo ndio ile siku ambayo madhehebu ya kumkomboa mtoto YESU yanafanyika, kwani yeye pia alikuwa mtoto wa kwanza.
         
Roho Mtakatifu anawaongoza wazee waliojaa imani katika kumtambua YESU na kumkiri kama kitulizo cha kiu yao. Nasi pia tukiongozwa na Roho wa Bwana, tuandamane twende katika nyumba ya MUNGU kumlaki KRISTO.

Ufafanuzi
         
Madhehebu matatu yalifuata baada ya uzazi wa mtoto wa kwanza wa kiume kati ya Wayahudi. Kwanza, baada ya siku nane mtoto anatahiriwa na kupewa jina. Pili, siku ya arobaini tangu kuzaliwa kwa mtoto kulikuwa na madhehebu ya kutakaswa kwa mama. Muda wote huo wa nyuma mama alihesabika kuwa ni mchafu kimadhehebu maana yake, alizuiliwa kushiriki katika matendo fulani ya kidini mathalani, kuingia hekaluni na kadhalika. Wakati wa kutakaswa alitoa sadaka, kondoo wa mwaka mmoja au njiwa wawili.
  
Madhehebu ya tatu ni kumkomboa mtoto. Watoto wote wa kwanza walihesabiwa kuwa ni mali ya MUNGU, wangetakiwa watumikie hekaluni. Ili kuwafanya watoto hao wawe tena mali ya wazazi wao, walipelekwa hekaluni na humo walifanyiwa madhehebu ya kuwakomboa. Wazazi walilipa shekeli 5 (aina ya sarafu ya fedha). Katika masimulizi yake, Luka anaunganisha madhehebu ya kutakaswa mama ma kukombolewa kwa mtoto. Kwa kweli Luka anaikariri tu sheria ya kumkomboa mtoto bila kusema waziwazi kuwa YESU alifanyiwa madhehebu hayo. Mkazo wake uko katika kutakaswa. Luka anataka kuwafundisha wasomaji wake mambo mawili muhimu. Kwanza, familia hii inazingatia barabara sheria za dini kama ilivyokwisha zingatia amri ya serikali hapo mwanzo. Pili, Luka anaonyesha umakini wa familia hiyo. Familia tajiri ilitakiwa kutoa kondoo wa mwaka mmoja wakati wa madhehebu ya kutakaswa  mama aliyejifungua mtoto wa kiume wa kwanza. YOSEFU na MARIA walitoa sadaka ya watu wenye uwezo mdogo, yaani njiwa wawili.
  
Ujio wa Familia Takatifu hekaluni ulileta furaha na ulikuwa ni nafasi ya kusikia makubwa juu ya mtoto YESU. Watu wawili, mwanaume na mwanamke walifurahi kumwona mtoto YESU aliye “faraja ya Israel”. Itakumbukwa kuwa MARIA alipomchukua mtoto YESU tumboni na kumtembelea Elizabeti ujio huo ulileta furaha kubwa katika nyumba ya Elizabeti.

Simeoni alikuwa mcha MUNGU maana yake alizingatia amri kiaminifu na maadili yake yalikuwa mema. Lakini, wala sheria za MUNGU, wala madhehebu mazuri ya Hekalu, hayakufanikiwa kukidhi haja ya Simeoni. Macho yaliangalia mbele siku ya ujio wa “faraja ya Israeli”. Faraja ya Israeli ni siku ya kuja kwake Masia atakayewafariji wana wa Israeli katika majonzi yao. Kwa jinsi hii Mwinjili anafundisha kuwa Agano Jipya ni bora zaidi kuliko Agano la Kale pamoja na sadaka zake zote. Simeoni anawakilisha watu walioweka matumaini yao kwa MUNGU, watu waliongoja kwa hamu kushuhudia wema wake MUNGU.
  
Kwa sababu ya uchaji wake kwa MUNGU, Simeoni alizawadiwa mambo matatu. Kwanza, kufika hekaluni siku hiyo hiyo mtoto alipotolewa. Pili, kumtambua huyo mtoto. Tatu, kujulishwa majukumu yake na matokeo ya kazi yake. Akiwa ameshika mtoto mikononi, Simeoni anaimba utenzi mfupi unaojulikana kwa maneno yake ya mwanzo ya lugha ya Kilatini “Nunc Dimitis”“Sasa Bwana waweza kumruhusu mtumishi wako”. Baada ya  kumwona mtoto huyo, Simeoni haoni kama kuna kitu cha maana zaidi kilichobaki katika maisha yake.

Mambo matatu muhimu yanasemwa juu ya mtoto YESU. Kwanza, ujio wake utaleta wokovu (mwanga) si kwa Waisraeli tu bali kwa watu wote. Injili ya Luka ni Injili ya Kimataifa. Pili, mtoto huyo atapitia mateso na kifo na hayo yatamletea mama yake mateso. Tatu, uwepo wa YESU utawalazimisha watu kufanya uamuzi wa dhati na wa kweli na sio nusu nusu au kuwa upande wake au kuwa dhidi yake. Nabii Isaya (8:14; 28:16) alitabiri mgawanyo huu wa watu utatokea baada ya kuja Masia.
         
Mcha MUNGU mwingine aliyeingojea faraja ya Israeli ni Bi Kizee  mjane nabii Anna. Mama huyu anaonyeshwa kuwa muhubiri wa Habari Njema, “Huyu alitoka saa ile ile akamshukuru MUNGU, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katila Yerusalemu akawatolea habari zake.”

Katika  maisha
Simeoni alimpokea mtoto YESU mikononi alisema, “sasa Bwana waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani.” Wewe unapopokea MWILI wa YESU  yaani Ekaristi Takatifu Sana, je, unajiona kweli umebahatika? Unaona kuwa hakuna kingine cha kukuletea faraja isipokuwa YESU peke yake?
Ili kufanikiwa katika maisha yetu ya kiroho, tunatahadharishwa na mafundisho ya KRISTO kwamba tusiweke matumaini yetu katika vitu vinavyoharibika kama vile mali, watu, magari (mashangingi). Hivyo vyote viwe ni kwa ajili ya  kutupeleka kwa YESU aliye faraja yetu ya pekee.    Yaani ni faraja yetu ya uhakika, ya kudumu, isiyoweza kuibiwa, na mchwa hawawezi kuiharibu. Kama ni hivyo basi tujipeleke kwa YESU bila kujibakisha, hata kama katika kumfuasa YESU tunakutana na mateso mengi na ya kuumiza. Tukivumilia yote hayo faraja yetu ni kubwa mno mbinguni. Tazama mama Bikira MARIA aliyevumilia mateso mengi kama mzee Simeoni alivyotabiri, yupo sasa mbinguni pamoja na YESU. Nasi pia tukikazana inawezekana kabisa.
         
Mafanikio yetu mbalimbali yasiwe sababu ya kushindwa kumuona YESU aliye kitulizo chetu. Mzee Simeoni pamoja na kuwa mcha MUNGU wa kuigwa, hakujidai chochote mbele ya YESU na binadamu wenzake. Tazama mimi na wewe wakati mwingine tunapofanikiwa katika hili au lile jinsi tunavyojidai na kupenda kujitenga peke yetu. Mzee Simeoni kwa vile hakuwa na mtindo huo alimtambua YESU mara moja.
 
 Fungua moyo wako leo ili YESU akutulize na majonzi uliyo nayo. Wewe mfungulie moyo tu naye atafuta machozi yako yote. YESU anayajua mahangaiko yako yote, anakusubiri umfungulie mlango wa moyo wako ili apate kuingia. Kazi yake ni kukufariji.

 Hitimisho
YESU KRISTO asiwe sababu ya mimi na wewe kuanguka bali awe sababu ya mimi  na wewe kuuona uso wa MUNGU. Yeye ni sababu ya kuanguka na kusimama kwa wengi. Tuuchukue Mwanga wa daima kama tulivyoibeba mishumaa nyumbani mwetu na hasa katika chumba cha ndani yaani moyo wako. Mwanga huo utakusaidia uione njia usianguke, uwaangaze majirani ili nao pia waione njia ile iongozayo katika uzima wa milele.

Post a Comment

 
Top