KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amesema kama kweli watu wanataka kuyafurahia maisha ya duniani, wanapaswa kufuata mambo kumi, anayoamini ni chanzo cha watu kukosa amani.

Anataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni kuzima televisheni, kuzitumia siku za Jumapili kwa kushinda na familia, na watu kuheshimiana kwa misingi ya dini, badala ya `kusilimisha’ wengine kutoka katika dini zao za asili. Katika mahojiano yaliyochapishwa katika gazeti la kila wiki la Argentina la `Viva’ Toleo la Julai 27 mwaka huu, amesema `Mambo Kumi’ anayoamini, yataibadilisha mno dunia.

Miongoni mwa mambo anayoshauri yafanyike ni wazazi kutenga muda wa kucheza na watoto wao, licha ya kubanwa mno na majukumu ya kimaisha, ikiwa pamoja na kazi.

“Hata kama wazazi wanafanya kazi kwa muda mrefu kiasi gani, wanapaswa kutenga muda wa kucheza na watoto. Kazi zinabana, lakini lazima watenge muda wa watoto,” anasema.

Aidha, alishauri siku za mapumziko ya Jumapili, ziwe maalumu kwa wanafamilia kuwa pamoja, badala ya kuhangaika na kazi, starehe kama pombe na `michepuko’ na mengine.

Papa huyo asiye na makuu, siku zote amekuwa akiwataka viongozi wa kiroho, kujishusha na kuishi maisha ya kawaida, badala ya anasa na kushindana kumiliki majumba na magari ya kifahari, akaunti zilizoshiba na mambo mengine kadhaa.

Pia, alishauri juu ya wanadamu kuacha kusengenyana. “Hata haya mambo ya kusemana, si mazuri hata kidogo. Yanachangia kuwafanya watu wajione dhalili, wajitenge kwa kudhani hawana thamani na matokeo yake wengine huishi kwenye ulevi hasa wa dawa za kulevya. Tunaiharibu dunia,” alisema.

Alisisitiza kuwa vijana wapewe nafasi ya kujiamini na kujaribu kuzichanga vyema karata za maisha yao, badala ya kuwakatisha tamaa. “Na katika imani, yafaa tuaminiane na kuheshimiana.

Haina sababu za kuikanyagakanyaga imani ya mwenzako na kumshawishi ahamie kwako, kwani unaathirika kwa kiasi gani kama mtu akibaki na imani yake?

Haya ya imani za watu pia ni chanzo cha machafuko, tuache watu wabaki na imani zao,” alisema Papa Francis, ambaye aliwahi kuwa mwalimu wa fasihi na mfanyakazi katika klabu ya usiku, kabla ya kuingia seminari.

Kanuni 10 za Kufurahia Maisha
Kwa mujibu wa Papa, `falsafa’ zifuatazo ndizo zinazoweza kumpa mtu uhuru na furaha.

1. ‘Ishi na acha uishi.’ Kila mtu anapaswa kuongozwa na kanuni hizi ambazo zinafanana usemi wa Roma unaosema, ‘Songambele na acha wengine wafanye hivyo pia.’

2. Ukarimu.‘Kuwa mtu wa kujitoa kwa wengine.’ Kama ukijifungia mwenyewe, kuna hatari utakuwa mbinafsi. Na maji yaliyotuama palepale, hugeuka kuwa mabaya.

3. ‘Endelea taratibu’ katika maisha. Papa alitumia taswira kutoka kwenye Kitabu kilichoandikwa na Ricardo Guiraldes, ambapo Mhusika Mkuu Don Segundo Sombra – anaangalia maisha aliyoishi nyuma.
Alisema katika ujana wake alikuwa kijito kilichojaa mawe mengi ambayo aliyabeba; kama mtu mzima, mto unaotiririka kwa kasi; na katika umri wa mzee, alikuwa bado anasogea, lakini taratibu kama kibwawa cha maji.
Alisema anapenda sehemu hiyo ya mwisho ya kibwawa cha maji-kuwa na ‘uwezo wa kusogea kwa upendo na ubinadamu, utulivu katika maisha.”

4. Burudani. Alisema ‘Furaha ya sanaa, fasihi na kucheza pamoja na watoto imepotea’. Alipendekeza familia zinapaswa kuzima televisheni wanapokaa kula- kuwasha `TV’ wakati wa kula kunazuia mazungumzo baina yenu, hivyo kuondoa ukaribu.

5. Jumapili. “Siku hizi zinapaswa kuwa siku za mapumziko. Wafanyakazi wanatakiwa wapumzike siku za Jumapili kwa sababu ‘Jumapili ni kwa ajili ya familia,” alisema.
Aliongeza kuwa, wapo wanaogeuza Jumapili kuwa siku za anasa kwa kutembelea kumbi za starehe, klabu za pombe na hata kujiachia na wapenzi wa nje.

6. Vijana. “Tafuteni njia za ubunifu kutengeneza ajira kwa ajili ya vijana. Tunahitaji vijana wabunifu. Kama hawana fursa watajitumbukiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya na kuwa hatarini zaidi kujiua,’alisema. ‘Haitoshi kuwapa chakula,” alisema. ‘Heshima unapewa, ukipeleka chakula nyumbani’ kutokana na kazi yake binafsi.

7. Heshimu Asili. “Uharibifu wa mazingira ni kati ya changamoto kubwa tulizokuwa nazo,” alisema. “Nafikiri swali ambalo hatujiulizi: Je, wanadamu hawajiui kwa kutumia maliasili kiholela na vibaya?”

8. Mawazo Chanya. Kuzungumzia wengine mabaya ni dalili za kutojithamini. Hiyo ina maana, “Najisikia niko chini, badala ya kujinyanyua mwenyewe, nataka kushusha wengine,” alisema Papa. “Kuachana na vitu hasi haraka ni kujijenga kiafya.”

9. Heshimu imani za wengine. “Tunawatia moyo wengine kwa ushuhuda wetu ili mkue wote kwa kuwasiliana. Lakini kibaya zaidi ni uongozi wa kidini, ambao hupoozesha. Nazungumza na wewe ili kukushawishi, Hapana.”

10. Amani. “Tunaishi katika kipindi chenye vita nyingi,” alisema. Aliongeza “Kelele za kutaka amani lazima zipigwe. Amani mara nyingine hutoa hisia ya kuwa kimya, lakini kamwe sio kukaa kimya, amani siku zote ni makini na nguvu.”

Post a Comment

 
Top