PADRE ni neno la Kiitaliano ambalo kwalo tunapata neno la Kiswahili Padri, maana yake kwa Kiswahili ni Baba. Kwa Kilatini Padre anaitwa Sacerdos. Jina hili linatoa mwanga zaidi juu ya maana na wajibu wa padre.

Jina Sacerdos limeundwa na maneno mawili ya Kilatini: “sacer”, hiki ni kivumishi kinachomaanisha kitu kitakatifu, na “dans” linatokana na kitenzi “dare” ambacho maana yake ni kutoa au kugawa. Kwa hivi tunaweza kusema kwamba Padre ni mgawaji wa Matakatifu.

Padri ni mtu mwenye kuheshimiwa na jamii si sana kwa sababu ya madaraka au umri wake, bali kwa kuwa anatarajiwa kuwa mtu mzima katika utume na huduma, kama jinsi Kristo alivyo Kuhani Mkuu si kwa umri wake wa kibinadamu, bali kwa ukamilifu wake wa Kimungu. Padri anakuwa pia Sacerdos kwa kuwa Kristo ni chemchem ambayo ndani yake Padri anachota matakatifu na anayagawa kwa wengine na bila shaka, yeye pia anajigawia yale yaliyo ndani ya uwezo wake.


Padri ni mtu muhimu na mwenye kuhitajiwa na kundi la watu wa Mungu. Kwa kinywa chake, anaweza kutamka maneno ya Bwana, “Mimi ni njia, ukweli na uzima. Hakuna ajaye kwa Baba ila kwa njia yangu mimi” (Yoh. 14:6). Padri ni Mtumishi wa Mungu anayejitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mungu. Ikumbukwe na kueleweka kwamba, “Kila Padri ni Kristo mwingine” ‘Alter Christus’. Pia “ni mwanadamu kama wanadamu wengine aliyetwaliwa kati ya watu na hupewa jukumu la kushughulikia mambo yamhusuyo Mungu kwa niaba ya watu, kutolea zawadi na dhabihu kwa ajili ya dhambi. 

Maadamu yeye mwenyewe ni dhaifu, anaweza kuwatendea kwa huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa. Kwa sababu hiyo anapaswa kutolea dhabihu si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe” (Ebr 5:1-3). Kumbe asiye binadamu hawezi kuwa Padri. Kwa hiyo Padri hata baada ya upadrisho anaendelea kuwa binadamu. Sote tunafahamu kuwa, hali ya kibinadamu ni hali ya unyonge, uchovu, kushawishika pamoja na kukata tamaa. Kwa hiyo si halali watu au Wakristo kukasirika wanapomwona padri mnyonge asiye kama Malaika.

Si halali kuwadai mapadri wetu kuwa na akili kama za Malaika, si halali kutaka upendo wao uyeyushe ugumu wa kila mkosefu au uwe na ufundi wa kutatua matatizo yote ya maisha. Ukweli ni kwamba wanaoteuliwa kuwa mapadri ni viumbe wanyonge wanaoshiriki unyonge wa ndugu zao. Hii inawawezesha kuwaombea ndugu zao bila unafiki. Vile vile tukumbuke kwamba, ni wajibu wa waamini wote kuwaombea mapadri wao ili waishi kadiri ya wito wao kwani “hakuna mtu ajitwaliaye heshima hii yeye mwenyewe, ila yeye aitwaye na Mungu kama alivyokuwa Aroni”. (Ebr 5:4). Tusikwazwe na unyonge wa Padri, bali kinyume chake kiwe ndicho ukweli.

Unyonge wa Padri uwe ni tumaini la wakosefu, uwe ni kitambulisho dhahiri kwamba Mungu hadharau unyonge wa binadamu. Mkosefu akikiri unyonge wake na kuomba msamaha Mungu atamjaza mema yake. “Wenye afya hawahitaji tabibu. Bali walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki au wema bali wenye dhambi” (Lk 5:31-32). Hayo ni maneno ya Kristo mwenyewe. Basi Padri kwanza ni binadamu kwa sababu ni mwakilishi na mwombezi wa kweli wa ndugu zake, hapa nikimaanisha taifa nzima la Mungu. Kwa hiyo inatubidi tushinde vishawishi vya kuwahukumu mapadri wetu, tuwaonee huruma, tuwaombee kama wanavyotuombea sisi na zaidi tuwaitikie mwito wao tuungane nao kwani ni wito wao kutuunganisha kwa jina la Kristo Bwana.

Yatubidi tufahamu kuwa padri yuko nasi katika kipindi cha kuzaliwa kwetu, kufa kwetu, wakati wa furaha na huzuni pia. Katika nyakati na sehemu muhimu za maisha yetu Padri yupo nasi. Mungu amempatia Padri uwezo mkubwa wa kuwatakatifuza watu. Sakramenti ya upadri iliwekwa na Kristo mwenyewe kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake pale alipowapatia wanafunzi wake Ekaristi Takatifu ambayo ingetolewa mpaka mwisho wa nyakati. Kazi hii huendelea kila siku katika ibada ya Misa Takatifu. Katika mlima wa mizeituni Kristo aliwapatia mitume uwezo wa kuondolea watu dhambi, kubatiza na kufundisha Habari Njema kwa watu wote. Padri anaendeleza wajibu huu yeye aliye mtume wa Kristo kwa mataifa yote.

Padri ana kazi ya kuwaelekeza watu kwa Mungu. Kwa uwezo aliopewa na Mungu, Padri hulinda roho za watu kwa chakula cha roho yaani Ekaristi Takatifu. Padri wa sasa huendeleza kazi ya mitume wa kwanza. Sakramenti ya upadri humfanya “Mkandidati” wa upadri kuwa kiumbe kipya na kumpatia alama isiyofutika, “Mwenyezi Mungu amekuapia wala hatabadili nia yake; wewe ni kuhani milele kwa utaratibu wa Ukuhani wa Melkisedeki” (Zab 110:4).

Kazi ya kwanza ya Padri kiujumla ni ya kiroho, yaani ya kutakatifuza watu. Kazi hii si ya siku moja, juma moja, miezi au mwaka, bali ni kazi ya kila siku mpaka wakati wa kifo chake. Kazi ya Padri ni ya wakati wote. Maisha ya Padri yameungana na Kristo na yametolewa kwa ajili ya watu wa Mungu. Tunamwita Padri “Father” au Abba, yaani Baba, na kweli ndivyo alivyo. Narudia tena Padri ni mwanadamu aliyepewa uwezo wa kutufanya watoto wa Mungu. Padri kweli ni mtumishi wa Mungu, lakini hata hivyo atakufa kama binadamu wengine. Kama Kristo mwingine hakuna mtu anayependwa sana na kuchukiwa sana kama Padri. Padri yuko katikati ya kila tatizo. Jitihada kubwa, kazi za ukarimu na sadaka mbalimbali vimekuwa majitoleo yake katika jumuiya.

Padri ni mtu wa ufahamu na mtu wa ukimya. Mtu anapoanguka kwa sababu ya ubinadamu husamehewa, lakini kwa padri ni tofauti; hupigiwa kelele na kuhukumiwa hapo hapo. (Jn 8: 7). Swali ni je! ni akina nani wanaomwona padri kuwa na kosa na kumuhukumu? Mara nyingi ni wale wale aliowasaidia kiaminifu na vizuri sana.

Mwandishi ni Frateri wa Seminari Kuu ya Mt. Karoli Lwanga- Segere, Jimbo Kuu Katoliki la Dar s Salaam anapatikana kwa simu namba 0686040044



Post a Comment

 
Top