KIFO NI HAKIKA
Jana nilikuwa kwenye Mazishi ya sista Dorothea Mkapuchini
huko MAUA MOSHI. Jana hiyo hiyo amefariki ndugu CHARLES CHISHIMBA
Mkapuchini wa Custos ya Zambia.
Katika nasaha alizotoa mkuu wa Shirika Nd. Wolfgang Pisa
OFMCAP ni tujenge utamaduni wa kukitafakari kifo. Mimi niliguswa sana na
ujumbe wake na hapa nimeonelea niwashirikishe ijapokuwa si wengi
mtaipenda hii Tafakari.
KIFO NI HAKIKA
Kwa maana u mavumbi wewe nawe mavumbini utarudi (Mwa 3:19)
Kila Jumatano ya Majivu Kanisa hutukumbusha ukweli kwamba
sisi ni mavumbi na mavumbini tutarudi. Siku inakuja ambapo mimi na wewe
hakika tutakufa. Hali hii inamsubiri kila mmoja wetu awe tajiri au
masikini, msomi au mjinga, mkleri au mlei, walio na nguvu au walio
dhaifu, walio wema na walio waovu. Ni wakati wa kifo, wakati ambapo roho
itauacha mwili, inaingia katika umilele, wakati mwili unarudia
mavumbini.
Kifo kinaweza kukutenda nini? Wakati wa maisha inawezekana
uliheshimika, ulifikiriwa, uliheshimiwa na kujienzi. Baada ya kifo mwili
wako unakuwa ni kitu ambacho ni lazima tuachane nacho mara kwani uozo
wake ni karaha kubwa. Ni lazima uzikwe haraka ukaingie katika zama za
wafu.
Wakati wa maisha inawezekana ulijulikana sana, watu
wakikuheshimu kutokana na busara zako, hekima, akili, uwepo wako na
ulihitajika sana.
Baada ya kifo haitachukua muda utasahaulika mara. Watu
watakaposikia juu ya kifo chako wengine wanaweza kusema: “Alikuwa mwema
kwa familia yake, kwa shirika lake.”
· Wengine watasikitika kwa sababu uwepo wako uliwafaidia –ndiye ulikuwa unawapatia mkate wa kila siku.
· Wapo wanaofurahia kifo chako kwa kuwa kwa uwepo wako ulikuwa unawawekea kiwingu.
Wakiamini kwamba kwa kutokuwepo kwako ni kwa faida yao
sasa. Lakini haitachukua muda kabla ya kusahaulika na hakuna
atakayeongea juu yako.
Kwa siku chache baada ya kifo chako, ndugu zako na marafiki
wako wa karibu watatetemeka watakaposikia jina lako wakiogopa kuibua
tena hisia za huzuni. Lakini haitachukua muda watafarijiwa, pengine hata
kwa wazo la kushiriki katika hali yako.
Kwa hiyo hata kwa wakati mfupi kifo chako kinaweza kuwa
sababu ya furaha, na katika nyumba yako, pengine katika chumba kile
ambapo ulifia, na kuhukumiwa na Yesu Kristo, wengine watafurahi na
kucheza, kula na kunywa, na kucheza kama ilivyokuwa kabla ya kifo chako.
Na roho yako itakuwa wapi?
Ndiyo maana unapaswa kukumbuka haya maneno ya ajabu:
“Kumbuka kwamba wewe ni mavumbi na mavumbini utarudi.” Mambo yana
mwisho, na ikiwa katika kifo utaipoteza roho yako, utakuwa umepoteza
kila kitu kwako.
Mt. Lawrence Justinian, anatukumbusha kuwa, unapaswa
kujiona mwenyewe kama ambaye amekwisha kufa, kwa kuwa unafahamu kuwa
hakika utakufa siku moja, na ni hivi punde. Aliongeza, na kama umekwisha
kufa, ni kipi ambacho usingalitamani kukifanya? Wakati unaishi kumbuka
kwamba siku moja utakuwa kati ya wafu kama mmoja wao.
Mt. Bonaventura anasema ili kuiongoza meli salama, nahodha
ni lazima daima abaki katika usukani. Kwa namna hiyo hiyo ili kuishi
maisha mazuri na yenye tija, ni lazima kujiona mwenyewe katika saa ya
kufa.
Wakati St. Camillus de Lellis alipopita makaburini na kuona
makaburi ya wale waliolala alijisemea mwenyewe: “Ikiwa watu hawa
wangaliweza kuishi tena, wangefanya nini ili waingie mbinguni? Ungefanya
nini, wewe ambaye bado unaishi na mwenye muda wa kujiandaa kwa siku ya
kifo yaani kumpokea dada mauti?
Kumbuka mfano ambao Yesu aliutoa kuhusu mtini usiozaa na
maneno aliyoyasema kwa mtunzaji wa mti ule: “Tazama miaka mitatu hii
naja nikitafuta matunda juu ya mti huu, nisipate kitu, uukate, mbona
hata nchi unaiharibu?” Lk 13:7
Umekuwa hapa duniani kwa zaidi ya miaka mitatu. Umezalisha
matunda ya aina gani mpaka sasa? Mt. Bernad anasema Bwana hafurahii tu
maua, ila pia matunda ambayo ni matokeo ya uwepo wa maua. Ndiyo kusema
kwamba Mungu hafurahii tu shauku yetu na ahadi tunazomwekea, ila zaidi
mno matendo mema ambayo tunayafanya tungali bado hai.
Jifunzeni kuutumia muda vizuri mngali hapa duniani.
Msisubiri mpaka muambiwe hakuna muda tena, au muda wa kuondoka hapa
duniani umekaribia. Jiwekeni tayari kufa hata sasa ikiwa ni mapenzi ya
Mungu. Kesheni kila wakati kwa kuwa hamjui saa.
Mwili kaburini
Ndugu yangu Mkristo, ili upate kutambua kile ulicho, nenda
makaburini ukatafakari ju ya kifo. Zingatia ushauri wa Mt. Yohani
Chrisostom: “Nenda kaburini, tafakari juu ya mavumbi, majivu, wadudu na
taka zilizopo humo. Hebu fikiri juu ya mzoga unavyojeuka kuwa njano
kisha kuwa mweusi.
Haichukui muda mwili wote utakuwa umejaa usaha mweupe,
wenye kutoa harufu kali ambayo hakuna anayependa kuivuta, fikiri juu ya
unene wa nyamba unavyosambaratika na kuacha mifupa, jinsi ambavyo mchwa
na wadudu wengine watakavyokuwa wanasherehekea kitoweo hicho. Hebu
fikiri juu ya panya wa kila aina ambavyo wanakimbilia chakula hiki,
wengine wakiingia midomoni na wengine tumboni na kwingineko kadiri
wanavyoweza.
Ni wakati ambapo kila kitu kinaanguka iwe nywele, mikono na
mengine. Mbavu zinaanikwa hadharani, kisha miguu na mikono inachomoka
kutoka kwenye mashiko yake. Mchwa kisha kula kila kitu, wanabaki
kushangaa mifupa ambayo pengine hawawezi sasa kuila, ni wakati ambapo
mifupa inaanza kutengana kule kushikana kwake, fuvu la kichwa linaachana
na kiwiliwili. Ama kweli mwanadamu si kitu. Huo ndio mwili unaokufa.
Tazama mtu ni nina! Ni kama mavumbi membamba yawezayo
kupeperushwa na upepo kidogo. Watazame watu maarufu, masharifu,
waliotawala mijadala mikubwa na kuonekana wamestawi kimaisha. Wamebaki
kuwa historia! Nao wamekufa wamelala makaburini. Makaburi ni makao yao
milele!
Walijijengea majumba makubwa, makasri, mahekalu, wakawa na
magari ya kifahari! Walivaa mavazi ya Hariri! Popote walipopita
waliheshimika sana! Walisalimiwa na kusujudiwa na watu! Leo hii wako
wapi? Ukitaka kujua ukweli wa maisha nenda makaburini! Huko ni uozo na
mifupa! Wamekuwa chakula cha sisimizi na siafu. Ee Mwenyezi Mungu, mtu
ni nini! Ingawa alisifika sana! Ingawa alijiinua sana! Alijipenda sana!
Alikuwa na watumishi wengi! Na kila alipopita alisujudiwa kutokana na
fedha zake! Cheo chake! Haiba yake! Leo hii yuko makaburini! Kimya
kabisa! Amegeuka kuwa chakula cha mchwa! Ama kweli binadamu hatadumu
katika fahari yake! (Zab 49).
Heri yenu ninyi watakatifu! Mlifahamu namna ya kutokuandama
na mwili na kama mlifanya chochote mliienzi roho yenu. Mliishi mkitoa
kipau mbele kwa Mungu ambaye kwa maisha yenu ya duniani mlimpenda kwa
kuwa ndivyo ilivyowapasa. Mlifunga ili kuunidhamisha mwili ili usiwe
kikwazo cha kumtumikia Mungu.
Kwa uaminifu wenu, sasa ingawa mlikufa kuhusu mwili mifupa
yenu sasa inaheshimiwa kama masalia matakatifu.mlielewa ukuu wa
mwanadamu na kwa sababu hiyo mliuzingatia ukweli wa maisha na sasa
mnafurahia heri ya mbingu, mkisubiri siku za mwisho ambapo miili yenu
itashiriki katika utukufu mtakaopewa kwa kushiriki maisha ya kristo
katika ulimwengu huu. Upendo wa kweli kuhusu mwili katika maisha haya ni
pamoja na kuunidhamisha, kufunga na kujikatalia hata starehe halali,
ili siku moja pamoja na roho yako mpokee tuzo ya heri ya milele.
Sala
Ee Mungu wangu, mimi ni sawa na ule mti ambao umestahili
kusikia maneno yale ya hukumu: “Ukate. Kwa nini unaendelea kuinyonya
ardhi?” Ndiyo Bwana mpaka sasa sijaweza kuzaa matunda yenye heri mbali
na miiba ya dhambi zangu.
Hata hivyo Bwana Mungu, si mpango wako niishi kwa kukata
tamaa. Umesema kwa wote wanaokutafuta watakupata: “Nitafuteni maadamu
ninapatikana.” Mt 7:7. Umesema pia” “Ninyi mkiomba lolote kwa jina
langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya mwana.” Yn 14:14.
Ee Yesu mwema na mpenzi wangu, nikijiaminisha katika ahadi
hizi zako, na katika jina lako na kwa mastahili yako, ninaomba neema na
upendo wako. Unijalie ili kwamba neema zako za kimungu na upendo wako
vitawale moyoni mwangu ambako hapo zamani dhambi ilitamalaki.
Bikira Maria mama yangu na mwombezi wangu, usikie kilio changu na uniombee kwa Yesu. Amina.
Post a Comment