KANISA LA MTAKATIFU FRANSISKO
KSAVERI
PAROKIA YA OLOSIPA
Parokia ya Mtakatifu Fransisko
Ksaveri ilianza kama Jumuiya ndogo ya wakristo wakatoliki mwaka 1998 ikiwa
sehemu ya Parokia ya Mtakatifu Mathiasi (Parokia ya
Ngaramtoni) na mwanzoni mwa mwaka 1999 Jumuiya hiyo ilizinduliwa
rasmi ikiwa na Jumla ya familia kumi zenye waamini ishirini na watano tu. Mnamo
Agosti 15, 1999 jumuiya hiyo ilifanya uchaguzi wake wa kwanza wa
kamati ya kudumu na wakati huo familia ziliongezeka kufikia kumi na tano
zenye waamini arobaini.
Kanisa la kwanza kujengwa kama kigango |
Kutokana na ongezeko hilo la
idadi ya waamini viongozi wa jumuiya hiyo kwa kushirikiana na aliyekuwa
Paroko wa wakati huo (Parokia ya Ngaramtoni) Padre Faustin Mosha,
walianza juhudi za kutafuta eneo la kujenga kanisa na bahati nzuri
mnamo tarehe 20 Septemba 1999, ndugu Meipusu (Peter) Kayan alilipatia
kanisa eneo lenye ukubwa wa meta 25 kwa meta 21 kwa ajili ya ujenzi wa
kanisa dogo ambao ulianza Novemba 16,1999, na ibada ya Misa
takatifu iliadhimishwa kwa mara ya kwenza kwenye kikanisa hicho na Padre
Faustin Mosha mnamo Desemba 27, 1999. Kanisa hilo dogo
lilibarikiwa na kuwa Kigango cha Parokia ya Ngaramtoni na Mhashamu Askofu Mkuu
Josaphat LEBULU tarehe 20 Aprili, 2000.
Kanisa la Mt. Fransisko Ksaveri |
Kati ya mwaka 2000 na
2006 Kikango kikiwa chini ya Paroko Padre Pastory Kijuu waamini walifanikiwa
kuongeza eneo la kanisa hadi kufikia ukubwa wa ekari 2.39 kwa ajili ya kujenga
kanisa kubwa lenye kukidhi waamini wengi. Kanisa kubwa lilianza kujengwa
Januari 2005 kwa hatua mbalimbali hadi 26-04-2011, lilipozinduliwa na
Kigango hicho kupewa hadhi ya Parokia na Padre Rochus Conrad Mkoba kuwa Paroko
wa kwanza wa Parokia ya Mt. Fransisko Ksaveri – Olosipa. Mwaka mmoja baadaye
tarehe 26-04-2012, kanisa liliwekwa wakfu (Kutabarukiwa) na Mhashamu Askofu Mkuu
Josaphat LEBULU.
Tangu kuanzishwa kwa Parokia
26-04-2011 hadi mwaka 2013 parokia ina jumla ya waamini wapatao 1,300, padre
mmoja mwanajimbo, ongezeko la Jumuiya toka 9 hadi 20, Vyama vya kitume toka
vitatu hadi 9, Mseminaristi mkubwa mmoja na waseminaristi wadogo 8, wasichana
wawili wako katika malezi ya utawa. Pia parokia ilifanikiwa kuchimba maji
yanayohudumia kaya 200, na kujenga ukuta kuzunguka eneo la kanisa na kuongeza
eneo la kanisa.
Changamoto
zinazozikabili
Parokia hii changa ni pamoja na ukosefu wa nyumba ya mapadre, (Padre
anaishi
katika nyumba ya kupanga)na miradi mbalimbali. Parokia inampango wa
kujenga nyumba ya mapadre, nyumba ya masista, zahanati, shule ya awali
na
msingi, ukumbi wa parokia na kuendelea kuongeza eneo ili kukidhi miradi
inayotazamiwa
kuanzishwa. Uongozi wa Parokia unakaribisha waamini na watu wote wenye
mapenzi mema kutoa michango yao ya hali na mali ili kuiwezesha Parokia
hii changa kupiga hatua kiroho na kimwili.