KANISA  LA MTAKATIFU FRANSISKO KSAVERI

PAROKIA YA OLOSIPA
Parokia ya Mtakatifu Fransisko Ksaveri ilianza kama Jumuiya ndogo ya wakristo wakatoliki mwaka 1998 ikiwa sehemu ya  Parokia ya Mtakatifu Mathiasi  (Parokia ya Ngaramtoni)  na mwanzoni mwa  mwaka 1999 Jumuiya hiyo ilizinduliwa rasmi ikiwa na Jumla ya familia kumi zenye waamini ishirini na watano tu. Mnamo Agosti  15, 1999 jumuiya hiyo ilifanya uchaguzi wake  wa kwanza wa kamati ya kudumu na wakati huo familia  ziliongezeka kufikia kumi na tano zenye waamini arobaini.
Kanisa la kwanza kujengwa kama kigango
Kutokana na ongezeko hilo la idadi ya waamini  viongozi wa jumuiya hiyo kwa kushirikiana na aliyekuwa Paroko wa wakati huo (Parokia ya Ngaramtoni) Padre Faustin Mosha,  walianza juhudi  za  kutafuta eneo la kujenga kanisa na bahati nzuri mnamo tarehe 20 Septemba 1999, ndugu Meipusu (Peter)  Kayan alilipatia kanisa eneo lenye ukubwa wa meta 25 kwa meta 21  kwa ajili ya ujenzi wa kanisa dogo ambao ulianza  Novemba 16,1999, na  ibada ya Misa takatifu iliadhimishwa kwa mara ya kwenza kwenye kikanisa hicho na Padre Faustin Mosha mnamo  Desemba 27, 1999.  Kanisa hilo dogo  lilibarikiwa na kuwa Kigango cha Parokia ya Ngaramtoni na Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat LEBULU tarehe 20 Aprili, 2000.
Kanisa la Mt. Fransisko Ksaveri
 Kati ya mwaka 2000 na 2006 Kikango kikiwa chini ya Paroko Padre Pastory Kijuu waamini walifanikiwa kuongeza eneo la kanisa hadi kufikia ukubwa wa ekari 2.39 kwa ajili ya kujenga kanisa kubwa lenye kukidhi waamini wengi.  Kanisa kubwa lilianza kujengwa Januari 2005 kwa hatua mbalimbali  hadi 26-04-2011, lilipozinduliwa na Kigango hicho kupewa hadhi ya Parokia na Padre Rochus Conrad Mkoba kuwa Paroko wa kwanza wa Parokia ya Mt. Fransisko Ksaveri – Olosipa. Mwaka mmoja baadaye tarehe 26-04-2012, kanisa liliwekwa wakfu (Kutabarukiwa) na Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat LEBULU.
Tangu kuanzishwa kwa Parokia 26-04-2011 hadi mwaka 2013 parokia ina jumla ya waamini wapatao 1,300, padre mmoja mwanajimbo, ongezeko la Jumuiya toka 9 hadi 20, Vyama vya kitume toka vitatu hadi 9, Mseminaristi mkubwa mmoja na waseminaristi wadogo 8, wasichana wawili wako katika malezi ya utawa. Pia parokia ilifanikiwa kuchimba maji yanayohudumia kaya 200, na kujenga ukuta kuzunguka eneo la kanisa na kuongeza eneo la kanisa.
Changamoto zinazozikabili Parokia hii changa ni pamoja na ukosefu wa nyumba ya mapadre, (Padre anaishi katika nyumba ya kupanga)na miradi mbalimbali.  Parokia inampango wa kujenga nyumba ya mapadre, nyumba ya masista, zahanati, shule ya awali na msingi, ukumbi wa parokia na kuendelea kuongeza eneo ili kukidhi miradi inayotazamiwa kuanzishwa. Uongozi wa Parokia unakaribisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoa michango yao ya hali na mali ili kuiwezesha Parokia hii changa kupiga hatua kiroho na kimwili.


Post a Comment

 
Top